Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira imeitaka Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA UWASA ) mkoani Tanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika baada ya kupata Sh54 bilioni katika mradi wa hati fungani zilizowekezwa na wadau.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Jackson Kiswaga kwenye ziara yao ya siku moja mkoani Tanga ya kutembelea vyanzo vya maji na kusema kuwa wananchi wanahitaji maji hivyo mamlaka husika ziwajibike kuboresha miundombinu.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso anasema wilaya ya Tanga mjini inapata maji kwa asilimia 95,ila wilaya ya Kilindi na Handeni bado upatikanaji wake wa maji haulidhishi kutokana na maeneo hayo kukosa vyanzo vya maji,huku maji ya ardhini yakiwa sio ya kutosha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa Mhandisi Geofrey Hilly anasema matarajio yao baada ya mradi huo kukamilika Tanga jiji itapata maji kwa zaidi ya asilimia 98 na kuwafikia wananchi zaidi ya laki sita.
Wilaya ambazo zitanufaika na mradi huo wa maji wa hati fungani utakapokamilika ni Tanga jiji,Muheza,Pangani na Mkinga.